KITUO CHA MWENDO KASI CHA POSTA NI GENGE LA VIBAKA.
Nilikuwa natoka shule mnazi mmoja kama saa sita kasoro jana jumapili tar 22/01/2017, kwa mwendo kasi nikashuka kituo cha posta cha mwendo kasi, ili niingie kazini kujisomea, sasa ninavyotembea pembeni ya ukuta wa Luther House, dereva wa guta barabarani akiwa ananipita akanisalimia halafu akaniambia, geuka nyuma kuna vijana wawili nyuma yako sio wazuri jiangalie sana. Sasa mimi nilivyotizama nikaona mmoja ana rasta na mwingine wa kawaida ni wa kawaida sana na ninawamudu lakini nyuma yao nikaona kama kuna kundi hivi. Wote wako umbali kama wa mita hamsini, nikaamua kutembea haraka hatua chache halafu nikavuka barabara ili niwapoteze, nao kwa wakavuka barabara pia ndipo nikavuka kurudi usawa nilipokuwa awali maana nilikuwa nimeshafika getini.
Wakati ninamsimulia mlinzi akaja kijana mmoja yuko na mountain bike anasema yeye ni msamaria mwema, akanieleza nina bahati sana lile kundi lote lilikuwa linakuja kwa ajili yangu. Nikajiuliza hivi amejuaje wakati mimi mwenyewe nimefanya kushtuliwa. Ndio hapo akasema vibaka wanadhani ndani ya hilo begi kuna laptop au video cameras na hivi una kitambi nimewachanganya. Nikamwambia hao wezi ni wapuuzi sana huku nikimfungulia begi nikamwambia nimetoka shule nakuja kujisomea kazini, nilichojaza humu ni madaftari tu. Akaangalia kwa kushtuka sana kana kwamba naye alikuwa na shauku ya kuona kilichomo. Nikamtilia mashaka bila kusema ila nilimkariri mavazi. Nikaingia ofisini nikasoma hadi saa kumi na moja ila wakati natoka walinzi wakanishauri niliache lile begi, nami nikatoka bila begi. Ninavyotoka nje ya geti sikuona mtu yeyote ninayemkumbuka wala kumjua ila wakati nimebakiza mita hamsini kufika kituo cha mwendo kasi hicho cha posta, hamad!! nikamwona yule msamaria mwema na mountain bike yake akiwa upande wa pili wa barabara akiendesha taratibu kana kwamba ananisindikizia mithili ya wale walinzi wa kisirisiri (Secret Service)
Nilichojifunza ndugu zangu ni hiki kifuatacho.
1. Usitembee njia yenye watu wachache hasa wakati wa weekend tena ukiwa na fedha nyingi au vitu vya kuvutia kama mabegi haya ya laptop, mabegi ya mgongoni hizi backpacks, simu na tablets.
2. Usipende kusimama kusaidia watu wanaotaka msaada kwako maana hao ni wapelelezi wa wezi kazi yao ni kutoa ishara tu uvamiwe.
3. Kuwa makini na watu walio pembeni yako na nyuma yako na kama kuna uwezekano weka umbali wa kutosha kama ni njia yenye watu wachache sana.
4. Acha mazoea ya kutembea usiku utakuwa wewe ndio umewaingilia wezi kwenye kazi yao.
Ukweli ni kuwa siku za weekend kuna vibaka katika njia zenye watu wachache. Kuweni makini sana sa hivi watu hawana hela vijana waliokata tamaa wameamua kuitafuta kwa nguvu, na wamejipanga vizuri wana roles na responsibilities hadi za ku-act kama decoy, wanajifanya wasamaria kumbe ndo wanakuangamiza.
No comments:
Post a Comment